WIZARA ya Maliasili na Utalii, inatarajia kuajiri maofisa misitu
1,000 mwaka wa fedha 2012/13 ili kupunguza uhaba wa maofisa hao nchini,
hivyo kukabiliana na vitendo vya uharibifu wa mazingira.
Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alitangaza neema hiyo katika mahafali ya Chuo cha Misitu Olmotonyi, wilayani Arumeru,
Mkoa wa Arusha.
Nyalandu alisema tatizo la ajira kwa maofisa
misitu, sasa litabaki kuwa historia hasa baada ya Serikali kuunda Wakala
wa Misitu, ambao hadi sasa ikama yao inahitaji wafanyakazi 2,500.
“Serikali
inathamini zaidi taaluma ya maofisa misitu, kwani ni muhimu katika
suala zima la utunzaji na uhifadhi wa misitu iliyopo nchini, ili kulinda
Tanzania isiwe jangwa, ajira za maofisa misitu zilikuwa zimesimamishwa
sambamba na ajira nyingine, lakini sasa zimerejeshwa,” alisema Nyalandu.
Alisema
hivi sasa hekta 90,000 za misitu ya uoto wa asili zinapotea kila mwaka
kutokana na ujangili wa misitu, biashara ya kuchoma mkaa na kuvunwa bila
utaratibu.
“Hivyo, ili kukabiliana na changamoto hizi, Serikali
inahitaji kuwa na maofisa misitu wa kutosha na tutawaajiri wahitimu wote
121 wa mwaka huu katika chuo hiki. Pia, tutawahitaji wahitimu 107 wa
mwaka jana na hata 101 wa mwaka juzi, wengine waliokuwa hawana ajira,”
alisema Nyalandu.
Kuhusu matatizo ya chuo hicho, Nyalandu alisema
wizara itajitahidi kuyafanyia kazi, ikiwamo kurekebisha mfumo wa uongozi
hivyo kukipa fursa ya kujiendesha na kuajiri walimu wake, ili kiweze
kupandisha madaraja kwa walimu na watumishi wengine kama vilivyo vyuo
vingine.
Hata hivyo, Nyalandu aliwataka wahitimu hao kutumia
taaluma hiyo vyema na kulisaidia taifa kukabiliana na changamoto za
mazingira, hivyo kuwa mabalozi wazuri wa chuo hicho katika soko la
ajira.
Awali, Mkuu wa chuo hicho, Christogunus Haule alisema
wanatoa mafunzo ya cheti na stashahada ya masitu, lakini kinakabiliwa na
changamoto mbalimbali ikiwamo uchakavu wa majengo, upungufu wa walimu,
bajeti isiyokidhi na na kuendesha propramu mbalimbali.
No comments:
Post a Comment