Sunday, January 15, 2017

Nia yetu ni kuhakikisha unapata bidhaa safi na bora kwa kuzingatia viwango vya utayarishaji wa vyakula nchini. Pata ASALI YA NYUKI WASIOUMA kutoka kwetu kwa ujazo na bei kulingana na uwezo wa mlaji

Thursday, August 18, 2016

Nyuki Mkombozi Co imekuletea mwonekano mpya wa usindikaji na ufungashaji wa ASALI MBICHI kutoka katika misitu ya hifadh ya miti ya ASILI Sikonge Tabora. Tunapokea order ya jumla na reja reja kwa wenye maduka madogo na makubwa. Wasiliana nasi kwa 0787 721 965 au 0752 155 830. Kwa Dar es Salaam duka letu lipo Sinza E mtaa wa Mamba teremka kituo cha White Inn au Kumekucha simu namba 0754 592 212 au 0756 550 000. Tumia ASALI HALISI ya Tanzania kutoka Nyuki Mkombozi Co. kupitia bidhaa yake bora ya FAHARI SWEET HONEY



Nyuki Mkombozi sasa inakuletea FAHARI SWEET HONEY na ipo madukani 

Sunday, September 1, 2013

MH MIZNGO PINDA ASEMA ZITAFUTWE MBINU ZA KUONGEZA UZALISHAJI WA MAZAO YA NYUKI TANZANIA.


 
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema jitihada zaidi zinatakiwa kufanyika ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya nyuki hapa nchini na kufikia angalau asilimia 50 ya uwezo ilionao wa kuzalisha tani 140,000 za asali na tani 10,000 za nta kwa mwaka.

“Mapori yote nchini pamoja na maeneo ya kilimo yana uwezo mkubwa wa kuzalisha mazao ya nyuki kwa wingi. Ushiriki wa sekta binafsi katika uzalishaji na uwekezaji katika viwanda bado ni mdogo hivyo nahimiza na kuamini kuwa ushiriki wa sekta binafsi ni chachu kubwa katika kukuza sekta hii ya ufugaji nyuki,” alisema.

Alitoa kauli hiyo jana jioni (Ijumaa, Agosti 30, 2013) wakati akizungumza wahitimu, wakufunzi na wazazi waliohudhuria mahafali ya kwanza na ya pili ya Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki cha Tabora yaliyofanyika kwenye viwanja vya chuo hicho.

Jumla ya wanafunzi 68 wamehitimu vyeti na stashahada ikiwa ni wahitimu wa mwaka 2011/2012 na 2012/2013 tangu kurejeshwa rasmi kwa mafunzo hayo kwenye chuo hicho cha Tabora kutoka Chuo cha misitu cha Olmotonyi kilichopo Arusha.

Waziri Mkuu alisema katika kipindi cha miaka minne iliyopita, kuanzia mwaka 2009 hadi 2012, uzalishaji wa asali hapa nchini ulifikia wastani wa tani 8,747 na wa nta ulifikia tani 583 kwa mwaka ambayo ni sawa na asilimia saba tu ya uwezo ambao nchi hii inao.

Alisema Tanzania ni moja kati ya nchi tano za Afrika zilizoruhusiwa kuuza asali yake katika soko la Umoja wa Nchi za Ulaya. Nchi nyingine ni Ethiopia, Zambia, Cameroon na Uganda. Alisema Ethiopia ndiyo inayoongoza kwa uzalishaji katika Afrika ikifuatiwa na Tanzania.

“Roho inaniuma ninaposikia kwamba Ethiopia ndiyo inaongoza kwa uzalishaji wa mazao ya nyuki barani Afrika. Wao wana jangwa kubwa tu, sisi tuna misitu kibao na maji ya kutosha. Lazima tujiulizie ni wapi tulikosea kwa sababu Tanzania ilikuwa inaongoza kwa uzalishaji kwenye miaka ya 60,” alisisitiza.

Ameutaka uongozi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki cha Tabora pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii wajipange na kuona namna ya kuinua uzalishaji huu. “Mkipata mitambo kidogo tu ya kusindika asali mtakuwa na nafsi kubwa ya kuwa wauzaji wakubwa wa asali nje ya nchi... wanunuzi wa nje wanataka traceability, ni rahisi kwa chuo kufanikiwa katika hili,” alisema.

“Soko lipo na bei nzuri. Tutumie fursa hii kuuza mazao yetu ndani na nje ya nchi ili kuongeza kipato cha kaya na cha Taifa kwa ujumla. Kama Asali inayozalishwa nchini itafungashwa vizuri kitaalam, kuna soko kubwa katika miji mikubwa, mahoteli, mashirika ya ndege, migodini na kwenye vituo vya utalii,” alisema.

Aliwataka wahitimu wa Chuo hicho watambue kwamba mafanikio katika maisha yao hayatategemea tu elimu ya ufugaji nyuki waliyojifunza, bali yatatokana na jinsi watakavyoitumia elimu hiyo kwa vitendo. “Elimu yenu ni zana, ni silaha, kwa hiyo itumieni vizuri. Ni silaha ya kuajiriwa, kujiajiri au kuwaajiri wengine katika miradi ya ufugaji wa nyuki, uzalishaji wa asali na nta na hatimaye kuleta maendeleo yenu binafsi na ya jamii nzima kwa ujumla,” aliwasihi.

Mapema, akitoa salamu za Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho, Kaimu Mwenyekiti, Bw. Liana Hassan aliiomba Serikali ikisaidie chuo hicho kupata sh. milioni 37/- ili kiweze kukamilisha mitaala yake kwa kuzingatia vigezo vya NACTE. Alisema kukamilika kwa hatua hiyo, kutakiwezesha chuo hicho kupata ithibati yake mapema.

Kuhusu changamoto zinazokikabili chuo, Bw. Hassan alisema miundombinu ya chuo haitoshi, madarasa hayatoshi, mabweni yamechakaa, na kwamba wanahitaji vifaa vya kisasa ili waweze kupata tarifa kupitia njia ya mtandao (internet).

Kuhusu tatizo la usafiri, Bw. Hassan alisema chuo kina gari moja tu ambalo ni la muda mrefu sana. “Tunaomba kupatiwa minibus mbili za wanafunzi, Land-Cruiser pick-up mbili ili zisaidie kubeba mahema na vifaa vingine wakati wanafunzi wakienda porini kimasomo na Land-Cruiser station wagon mbili kwa ajili ya idara ya utawala,” alisema.

Wakati huohuo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Bibi Fatma Mwassa wakati akitoa salamu za mkoa huo kwa wahitimu aliwaasa wasisubiri kazi za kuajiriwa bali wafikirie kujiajiri kwani mafunzo waliyohitimu yanawapa fursa hiyo. Alitoa ofa ya mizinga ya nyuki kwa vijana 10 wa kutoka Tabora watakaojiunga pamoja na kuamua kuanzisha manzuki (apiary) yao ili kujiletea maendeleo.

 

Tuesday, May 14, 2013

Wafugaji wa nyuki wa Wilaya ya Hanang’ Mkoani Manyara wametakiwa kutumia fursa za soko la asali toka kampuni ya Honey King ya mjini Kibaha mkoani Pwani kwa kujinyanyua kiuchumi.


Hayo yalisemwa jana tarehe 04/04/2013 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji) Dk Mary Nagu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Hanang’ kwenye uhamasishaji wa vikundi vya ujasiriamali wa ufugaji wa nyuki wilaya ya Hanang. Dk Nagu alisema vikundi 13 kupitia vyama vyao vya kuweka na kukopa (Saccos) wataweza kujinufaisha kimaendeleo kwa kujiwezesha kiuchumi pindi wakitumia fursa hiyo ya kuwepo na soko la uhakika la asali kupitia Honey King. Alisema wadau hao wa ufugaji wa nyuki wanatakiwa kujipanga,kwani shughuli za ufugaji wa nyuki hazihitaji gharama kubwa na pia soko la asali siyo tatizo tena kwani halihitaji kutafutwa lipo karibu na kwa uhakika. Aliwataka vijana wengi zaidi wa wilaya hiyo kujiunga kwenye vikundi na kuchangamkia fursa hiyo kwa kufuga nyuki,ambazo zitawapatia asali ya kutosha na kuondokana na umasikini kwenye jamii zao. Naye,Mratibu wa kampuni ya Honey King Filbert Sanka,alisema soko lao lina uwezo wa kununua tani 300 za asali hivyo wajasiriamali wa wilaya hiyo waitumie kwa kuhakisha wanakusanya asali ya kutosha na kuwauzia

Thursday, February 7, 2013

PINDA ATUNUKIWA TUZO YA HESHIMA BORA NA UFUGAJI WA NYUKI 2012




WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ametunukiwa  Tuzo ya Heshima ya Mwaka 2012 ya Mkoa wa Katavi katika vipengele viwili vya Utawala Bora na Uhamasishaji wa ufugaji nyuki.

Waziri Mkuu alipokea tuzo hizo, kwenye hafla ya kuuaga mwaka 2012 na kuukaribisha mwaka 2013 iliyofanyika kwenye ukumbi wa Idara ya Maji mjini Mpanda,
Akitoa maelezo ya utangulizi kabla ya kutangaza majina ya watunukiwa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Mhandisi Emmanuel Kalobelo alisema mkoa wa Katavi umeamua kuanzisha mfumo wa utoaji wa Tuzo ya Mkoa kwa lengo la kuwatambua, kuwatia moyo na kuwapa motisha wananchi na watumishi wa umma waliofanya vizuri katika nyanja mbalimbali za utoaji wa huduma kwa wananchi.
  
Sekta zilizopewa tuzo ni mapato na kodi za Serikali, utawala bora, uchumi na maendeleo, Ulinzi na usalama, mipango miji, mawasiliano na teknolojia, ufugaji nyuki na hifadhi ya mazingira, elimu, kilimo na mifugo, michezo, usafirishaji na huduma za jamii.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda anatunukiwa tuzo ya utawala bora, siasa safi na ushiriki katika shughuli za maendeleo ya wananchi wa jimbo lake la Katavi na Ukanda wa Ziwa Tanganyika kikamilifu.

 Mhandisi Kalobelo amesema Tuzo hiyo  itaendelea kutolewa kila mwisho wa mwaka ambapo wameamu kufanya hivyo  ili kuamsha ari kwa wengine kufanya vizuri zaidi mwaka unaofuata.


Sunday, September 9, 2012

SERIKALI KUAHIDI AJIRA 1000 KWA MAAFISA MISITU.

WIZARA ya Maliasili na Utalii, inatarajia kuajiri maofisa misitu 1,000 mwaka wa fedha 2012/13 ili kupunguza uhaba wa maofisa hao nchini, hivyo kukabiliana na vitendo vya uharibifu wa mazingira.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alitangaza neema hiyo katika mahafali ya Chuo cha Misitu Olmotonyi, wilayani Arumeru, Mkoa wa Arusha.
Nyalandu alisema tatizo la ajira kwa maofisa misitu, sasa litabaki kuwa historia hasa baada ya Serikali kuunda Wakala wa Misitu, ambao hadi sasa ikama yao inahitaji wafanyakazi 2,500.
“Serikali inathamini zaidi taaluma ya maofisa misitu, kwani ni muhimu katika suala zima la utunzaji na uhifadhi wa misitu iliyopo nchini, ili kulinda Tanzania isiwe jangwa, ajira za maofisa misitu zilikuwa zimesimamishwa sambamba na ajira nyingine, lakini sasa zimerejeshwa,” alisema Nyalandu.
Alisema hivi sasa hekta 90,000 za misitu ya uoto wa asili zinapotea kila mwaka kutokana na ujangili wa misitu, biashara ya kuchoma mkaa na kuvunwa bila utaratibu.
 “Hivyo, ili kukabiliana na changamoto hizi, Serikali inahitaji kuwa na maofisa misitu wa kutosha na tutawaajiri wahitimu wote 121 wa mwaka huu katika chuo hiki. Pia, tutawahitaji wahitimu 107 wa mwaka jana na hata 101 wa mwaka juzi, wengine waliokuwa hawana ajira,” alisema Nyalandu.
Kuhusu matatizo ya chuo hicho, Nyalandu alisema wizara itajitahidi kuyafanyia kazi, ikiwamo kurekebisha mfumo wa uongozi hivyo kukipa fursa ya kujiendesha na kuajiri walimu wake, ili kiweze kupandisha madaraja kwa walimu na watumishi wengine kama vilivyo vyuo vingine.
Hata hivyo, Nyalandu aliwataka wahitimu hao kutumia taaluma hiyo vyema na kulisaidia taifa kukabiliana na changamoto za mazingira, hivyo kuwa mabalozi wazuri wa chuo hicho katika soko la ajira.
Awali, Mkuu wa chuo hicho, Christogunus Haule alisema wanatoa mafunzo ya cheti na stashahada ya masitu, lakini kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo uchakavu wa majengo, upungufu wa walimu, bajeti isiyokidhi na na kuendesha propramu mbalimbali.